Ijumaa, 11 Desemba 2015

HISTORIA YA DR. LIVINGSTONE KWA LUGHA YA KISWAHILI




HISTORIA YA DR. LIVINGSTONE HAPA UJIJI
SAFARI ZA DR. LIVINGSTONE HUKU AFRIKA
Dr. David Livingstone alizaliwa huko Blantyre, Uskochi tarehe 19/03/1813. Dr. Livingstone alisoma masomo ya udaktari wa binadamu katika chuo kikuu cha Cambridge. Alifanya safari za kuja Afrika mara tatu kwa nyakati tofauti. Safari yake ya kwanza alikwenda Afrika ya kusini mwaka 1841. Alikutana na Robert Moffat ambaye alikuwa akiishi huko. Mwaka 1843 Dr. Livingstone alioa binti wa Robert Moffat (Mary). Walifanikiwa kupata watoto watatu ambao wawili walikuwa ni wa kiume na mmoja wa kike. Kwa bahati mbaya, ilipofika mwaka 1852 mke wa Livingstone alifariki dunia kwa ugonjwa wa Malaria huko Chupanga, Msumbiji. Dr. Livingstone aliwapeleka watoto wake Ulaya kwa ajili ya masomo.

Mwaka 1859, Dr. Livingstone alifanya safari yake Afrika kwa mara ya pili. Dr. Livingstone alikuwa mzungu wa kwanza kuona maporomoko ya Victoria na mto Zambezi katika ukanda wa Afrika ya kusini. Baada ya uvumbuzi huo, Dr. Livingstone aliamua kurudi kwao Uingereza ili aweze kutoa hotuba yake katika chuo kikuu cha Cambridge juu ya uvumbuzi huo. Katika hotuba yake hiyo aliwahamasisha wazungu wenzake kuja katika bara la Afrika kufungua njia za biashara na kueneza dini ya kikristu.

Ilikuwa ni mwaka 1866 ambapo Dr. Livingstone alikuja Afrika kwa mara ya tatu. Lengo la safari yake ilikuwa ni kuchunguza chanzo cha mto Nile. Safari yake ilianzia katika chanzo cha mto Ruvuma, Mikindani Mtwara. Alifuata huu mto mpaka ziwa Nyasa, Banguela na Mweru. Dr. Livingstone alifika mpaka kwa wamanyema (Zaire). Alikuta biashara ya watumwa ikiwa imeshamiri sana na ilikuwa ikiendeshwa na Waarabu pamoja na Waswahili. Dr. Livingstone alivuka maji ya ziwa Tanganyika na kufika Ujiji kwa mara ya kwanza mwaka 1869 ambapo aliweka kambi ya muda mfupi. Mji wa Ujiji ulipata maarufu kwa sababu ya biashara ya watumwa. Watumwa wengi walikuwa wakikamatwa huko Zaire na Burundi na kuletwa Ujiji ili waweze kusafirishwa kutoka Ujiji mpaka Bagamoyo. Watumwa hao walikuwa wakisafirishwa kupitia njia ya kati ya watumwa ambayo mpaka sasa kuna ushaidi wa miti ya miembe iliyokuwa imeoteshwa na waarabu.

HOFU YA KIFO CHA DR. LIVINGSTONE
Kwa kipindi cha miaka mitano (1866-1871), Dr. Livingstone hukufanya mawasiliano yoyote na serikali yake ya Uingereza. Hali hii ilizua hofu huko Ulaya kwamba huenda Livingstone alikuwa ameshakufa huku Afrika. Katika kipindi hichi afya ya Dr. Livingstone ilikuwa imedhoofika sana kwani alikuwa akiugua ugonjwa wa Malaria mara kwa mara, na alikuwa akisubiri kifo chake.

UJIO WA HENRY MORTON STANLEY
Wazungu wengi sana huko Ulaya waliamini kuwa Dr. Livingstone amekufa lakini mhariri wa gazeti la New York Herald James Gordon Bannett (Jnr) hakuamini habari hizo za kifo cha Dr. Livingstone. Mhariri huyu aliamua kumtuma ripota wake mahiri Henry Morton Stanley kuja kumtafuta Dr. Livingstone huku Afrika. Stanley alikuwa ameajiriwa huko Marekani katika gazeti la New York Herald ingawa utaifa wake ulikuwa ni wa Uingereza.
Stanley alifika Zanzibar tarehe 6/1/1871. Baada ya kufanya maandalizi kwa muda wa miezi miwili ya kumtafuta Dr. Livingstone. Ilipofika mwezi wa tatu mwaka 1871 alifika Bagamoyo.

KUKUTANA KWA STANLEY NA DR. LIVINGSTONE CHINI YA MTI WA MWEMBE
Ilikuwa tarehe 10/11/1871 ambapo Stanley alikutana na Dr. Livingstone kwa mara ya kwanza hapa Ujiji. Stanley na Livingstone walikaa kwa pamoja kwa muda wa miezi mnne katika eneo la Ujiji na Kwihara Tabora. Pia Stanley alishiriki safari za Dr. Livingstone haswa katika ukanda wa kaskazini mwa ziwa Tanganyika. Stanley alimshawishi Livingstone arudi kwao Uingereza lakini Dr. Livingstone alikataa.

Tarehe 14/03/1872 Stanley alikwenda pwani ya bahari ya Hindi na alifika Bagamoyo tarehe 6/5/1872. Siku iliyofuata alikwenda Zanzibar na tarehe 19/5/1872 alifika Uingereza. Ilipofika tarehe 1/8/1872 aliandaa hotuba mbalimbali ambazo zimemfanya awe maarufu sana duniani hadi leo.

UMAARUFU WA MTI MKUBWA WA MWEMBE
Chini ya mti huu wa mwembe ndipo Dr. Livingstone na Stanley walikutana kwa mara ya kwanza hapa Ujiji. Mti huu uliishi mpaka miaka ya 1920’s. Lakini katika kipindi hicho mti huo ulikuwa umeanza dalili za kuanza kudhoofika. Kutokana na umaarufu wa mti huu wa mwembe, serikali ya kikoloni ya mwingereza haikutaka mti huu upotee, ndipo ilipoamua kukata matawi manne ya mti huu na kuyapandikiza. Hivi leo kuna miti miwili ya maembe iliyopandikizwa. Baada ya mti huu wa mwembe kufa kuliamuriwa kujengwe mnara ili uwakilishe mti huu wenye historia ya kipekee. Mnara huu ulijengwa mwaka 1927 chini ya serikali ya mwingereza.

KIFO CHA DR. LIVINGSTONE
Mwezi wa nane, mwaka 1872 Livingstone alikwenda Chitambo, Zambia na alikufa huko tarehe 1/5/1873. Watumishi wake wanne Susi, Chuma, Mumwaswere na Uchopere waliufanyia upasuaji mwili wa Livingstone na kumtolea utumbo, maini na moyo na kuviweka katika sanduku la chuma na kulifukia chini ya mti wa Mvule. Pia waliupaka mwili wa Livingstone chumvi na viungo vingine ili usiharibike. Walianza safari yao kutoka Chitambo, Zambia mpaka Bagamoyo ambapo mwili wake ulipokelewa na wamissionari. Wamissionari waliufanyia misa takatifu na kuusafirisha kwenda Uingereza kupitia Zanzibar. Tarehe 15/4/1874 mwili wa Dr. Livingstone ulizikwa katika makaburi ya Westminster Abbey.

MAMBO ALIYOYAFANYA DR. LIVINGSTONE HUKU AFRIKA
        i.            Dr. Livingstone alikuwa akipeleleza Afrika juu ya tamaduni za waafrika, rasilimali zake na kuzitolea taarifa katika taifa lake la Uingereza.
      ii.           Dr. Livingstone alieneza dini ya kikristo katika maeneo ya ndani ya Afrika.
    iii.          Dr. Livingstone alikomesha biashara haramu ya watumwa. Alikuwa akinunua watumwa kwa kutumia pesa yake na kuwaachia huru, kwani Chuma na Susi walikombolewa katika biashara hii haramu ya utumwa na Dr. David Livingstone.

Imeandaliwa na:
Kelvin Ngowi,
Mhifadhi wa Mambo ya Kale,
Makumbusho ya Dr. Livingstone,
S. L. P. 565, 
Ujiji-Kigoma, Tanzania.
0766014335, 0712207460
ngowike91@gmail.com




p


Maoni 9 :

  1. I really liked as a part of the article. With a nice and interesting topics
    stanely and livingstone

    JibuFuta
  2. Thank you Bharath and we hope that you will visit Dr. Livingstone Museum in Ujiji Kigoma.

    JibuFuta
  3. Naomba kujua mzungu alieandika mateso na madhara ya biashara ya utumwa

    JibuFuta
  4. Nimefurahi sana kupata taarifa ya Dkt.David Livingstone

    JibuFuta
  5. Naitaji kujua ndugu zake

    JibuFuta
  6. Nimefurahia historia ya Dr Livingstone na huduma yake ya injili pamoja na huruma yake ya kununua watumwa na kuwaachia huru.

    JibuFuta
  7. Nimevutiwa na huduma ya kueneza injili ya Dr Livingstone pamoja na kuwanunua watumwa na kuwaachia huru.

    JibuFuta